Sitta aitaka Serikali kuleta uhuru wa habari

Sitta

Na Faraja Mgwabati

SPIKA wa Bunge la Tanzania, Samuel Sita ametoa mwito kwa Serikali kuwasilisha Miswada ya Sheria zinazokinzana na dhana ya uhuru wa habari nchini ili kuongeza ufanisi wa utendaji wa vyombo vya habari.

Akifungua Mkutano wa Siku ya Vyombo vya Habari uliofanyika Dar es Salaam jana, Sitta alisema pamoja na hatua kubwa iliyopigwa, Tanzania kama ilivyo kwa nchi nyingi bado ina safari ndefu kufikia uhuru kamili wa vyombo vya habari.

Alisema kwa mfano, Sheria ya magazeti ya 1976 inampa Waziri mwenye dhamana ya habari kuvifungia vyombo vya habari huku sheria ya Usalama wa Taifa ya 1995 nayo inatoa mamlaka kwa Serikali kuingilia shughuli za vyombo hivyo pale vinapotoa habari zinazodhaniwa kuwa ni za kuhatarisha Usalama wa Taifa.

“Natoa wito kwa Serikali kuziwasilisha Bungeni Sheria zinazolalamikiwa ili ziweze kufanyiwa marekebisho na binafsi naahidi kuunga mkono jitihada zote zitakazoleta uhuru wa vyombo vya habari.

Hii ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba bila kuchelewa zaidi kwa Miswada ya Sheria za Haki ya Kupata habari na Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari inaletwa Bungeni na kujadiliwa,” alisema Sitta katika mkutano ambao uliandaliwa na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika tawi la Tanzania (MISA-TAN).

Spika alisema hatahivyo wanahabari lazima wakumbuke kuwa upatikanaji wa uhuru kamili vyombo vyao ni mchakato ambao wadau wake wakubwa ni wanahabari wenyewe kwakushirikiana na wanaharakati wa haki za binadamu na wananchi kwa ujumla.

“Hivyo hamna budi kwa njia ya majadiliano kuendelea kuishinikiza Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine ili ione umuhimu wa kuzifuta au kuzifanyia marekebisho ya sheria zinazolalamikiwa,” alisema Sitta.

Sitta aliwataka waandishi nao kufuata maadili ya taaluma ya Uandishi wa habari katika utekelezaji wa majukumu yao ama sivyo itakuwa ngumu kufikia ndoto ya kuwa na uhuru kamili wa vyombo vya habari.

“Nawasihi waandishi wa Habari tuzingatie miiko ya upashanaji habari. Tuepuke kuingiza chuki, uongo na ubinafsi katika taaluma na zaidi nawaomba wanahabari kukataa kutumika na wanasiasa na matajiri ili kutoa habari zisizo na tija kwa nchi yetu. Mtaheshimika pale tu na nyinyi mtajiheshimu na kuenzi taaruma yenu,” alisema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa MISA-TAN, Ayub Ryoba aliishauri Serikali kulitumia zaidi Baraza la Habari Tanzania (MCT) katika kutatua mambo mbalimbali badala ya kukimbilia kuvifungia vyombo vya habari.

End

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s


%d bloggers like this: