Mabomu mengine Mbagala Dar es Salaam Mei 7

Mabomu

Faraja

JESHI la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) leo kuanzia saa tisa alasiri litalipua masalia ya mabomu yaliyobaki katika mlipuko uliotokea Aprili 29 mwaka huu ili kuepusha uwezekano wa mabaki hayo kuleta madhara zaidi.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa ulipuaji huo utafanyika katika Kambi ya JWTZ iliyopo Mbagala, eneo ambalo mabomu ya awali yalilipuka.

Dk. Mwinyi alisema kazi hiyo itafanywa na wataalamu wa Jeshi na hakutakuwa na madhara yeyote kwa watu kwani yatalipuliwa kiufundi. Lakini alisema watu itabidi kuanzia muda huo wakae mita 500 kutoka eneo la Kambi hiyo.

Waziri amewatoa wasiwasi wananchi wa Dar es Salaam hasa wale wa Mbagala kuwa zoezi hilo litafanyika kwa umakini kwa utaratibu wa kutanguliza milipuko miwili midogo kwa ajili ya kutoa tahadhari.

“Kisha baada ya milipuko hiyo miwili, itafuatia milipuko mingine ya mfululizo ya nguvu kiasi hadi saa 11 jioni…wananchi wanaombwa wawe umbali wa mita 500 kutoka kambi ya Mbagala,” alisema Mwinyi.

“Vilevile Wizara ya Ulinzi na JKT inapenda kuwahakikishia wananchi kwamba kazi hiyo itafanyika kwa uangalifu mkubwa na kwa usalama,” alisisitiza Waziri Mwinyi.

Mwinyi alisema silaha zitakazoharibiwa ni pamoja na masalia ya risasi, baruti, viwashio na mabomu ambayo hayakuweza kulipuka siku ilipotokea ajali.

Alisema jumla ya mabomu 75 ya kutupa kwa mkono aina ya Stick hand grenades na dazeni kadhaa za viwashio pamoja na fyuzi zake zitateketezwa.

Alisema mabomu hayo inabidi yaharibiwe eneo hilo kwa sababu yanaweza kulipuka wakati wa kuyahamisha na kuleta madhara kwa watu watakao yahamisha.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, John Lukuvi alisema wananchi waendelee na kazi zao kama kawaida kwani zoezi hilo halitaweza kuingilia kazi za watu.

Lukuvi alisema hata wanafunzi waendelee kwenda shule kama kawaida na kusitokee kisingizio chochote cha wanafunzi au watu kushindwa kwenda kwenye shughuli zao au shuleni.

Naye Mkuu wa Usalama wa JWTZ, Brigedia Generali Paul Mella alisema kambi ya Mbagala ina wanajeshi 200 ambao watasaidia kuwaelekeza wananchi kabla ya ulipuaji wa mabomu kuanza.

End

Leave a comment